Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania wote kuibua taarifa zinazohusu vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) leo tarehe 20 Januari 2025.
Amesema wapo wanawake, watoto na wanaume wanaopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawatoi taarifa kwenye vyombo vya sheria, vilevile baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikitumika kuwakandamiza waathirika.
Amesema pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha usawa wa kijinsia hapa nchini, bado wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watu hapa nchini, wanapewa nafasi ndogo katika umiliki wa mali na wanabaguliwa kwa msingi wa jinsia.
Aidha mesema dhamira hiyo ya Serikali inaonekana zaidi kupitia mikakati, mipango na sera za kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (NSGR) na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2000.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Juma amewataka wataalamu hao washeria Kuona ni kwa namna gani wanaitumia dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Hadi 2050 katika kubadili Mfumo unaowanyima haki za kisheria wanawake .
Naye Mwenyekiti wa chama cha Majaji wanawake Tanzania TAWJA Jaji Barke Sehel amesema mafanikio waliyopata nikutokana na uwepo wa mifumo ya usawa na jinsia hapa Nchini hivyo watahakikisha wanapambana ili kutokomeza vitendo vya ukatili.
Leave a Reply