Serikali Kujizatiti Kulinda Haki za Walimu Nchini

Serikali ya Tanzania imesisitiza azma yake ya kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya watumishi wa umma ambao wamekuwa kikwazo kwa walimu nchini, hasa walimu wanawake. Kauli hii imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobasi Katambi, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Walimu Wanawake Taifa.

Mhe. Katambi amesema kuwa serikali haitamvumilia mtumishi yeyote wa umma anayewanyanyasa au kuwatengenezea mazingira magumu ya kazi walimu, hususan wanawake. Ameongeza kuwa wale wanaoleta changamoto hizo watakabiliwa na hatua kali za kisheria.

“Kama yupo mtu kwenye ofisi ya umma ambaye atanyanyua mabega anajifanya Mungu mtu, anataka kutukuzwa na kuleta mazingira magumu kwa walimu wangu wa kike, hao wafikishwe kwa Mama Samia,” alisema Mhe. Katambi kwa msisitizo.

Pamoja na kutoa onyo hilo, Mhe. Katambi aliipongeza Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kazi nzuri ya kuhakikisha utulivu miongoni mwa walimu na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi. Alisema kuwa ushirikiano wa CWT na serikali ni muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu kote nchini.

Hatua hii ya serikali inalenga kuimarisha mazingira ya kazi kwa walimu, ambao ni msingi wa maendeleo ya elimu nchini. Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha walimu wanatekeleza majukumu yao katika mazingira salama, yenye heshima, na usawa wa kijinsia.