Maradhi ya Moyo yachangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza

Dodoma, Tanzania – Magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka kwa kasi duniani, yakisababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 17 kila mwaka, huku maradhi ya moyo yakitajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa za ongezeko hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Dkt. Kisenge alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, JKCI imefanikiwa kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo, uchunguzi wa kina, na tiba za kisasa.

Amebainisha kuwa maradhi ya moyo yamekuwa yakichangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kiharusi, na kisukari. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kubadili mtindo wa maisha kwa kula lishe bora, kufanya mazoezi, na kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi.

Kadhalika, Dkt. Kisenge ametoa wito kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa afya, mashirika yasiyo ya kiserikali, na sekta binafsi kushirikiana katika kupambana na magonjwa haya ili kupunguza mzigo wa kiafya kwa jamii na taifa kwa ujumla.