Dar es Salaam – Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu mfanyabiashara Hamis Said Luwongo adhabu ya kifo kwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa, Naomi Marijani.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Februari 26, 2025, na Jaji Hamidu Mwanga baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi 14 pamoja na vielelezo 10 vilivyowasilishwa mahakamani.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Yasinta Peter, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Ashura Mnzava, ulidai kuwa mshtakiwa alimuua mkewe kwa makusudi, hivyo akaomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
“Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili mkubwa na kinatishia usalama wa wanawake waliopo kwenye ndoa na wale wanaotarajia kuingia kwenye ndoa. Tunaomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe mfano kwa wanaume wanaotumia ndoa kama kisingizio cha kufanya ukatili,” alisema Wakili Mnzava.
Mahakama ilizingatia hoja hizo na kuona kuwa ushahidi uliotolewa unathibitisha bila shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorekebishwa mwaka 2019.
Kutokana na hukumu hiyo, mshtakiwa anatarajiwa kutumikia adhabu yake kwa mujibu wa sheria, huku hukumu hiyo ikitazamiwa kuwa fundisho kwa jamii kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Leave a Reply