Darasa Laporomoka Same, Wanafunzi 30 Wanusurika

Wanafunzi 30 pamoja na mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Tumaini Jema, iliyopo wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, wamenusurika kifo baada ya jengo moja la darasa walilokuwa wakisomea kuanguka kutokana na upepo mkali.

Wanafunzi hao pamoja na mwalimu wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Same, ambapo hali zao zinaendelea kuimarika.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, akiambatana na Kamati ya Usalama ya wilaya, amefika katika shule hiyo na kusimamisha shughuli zote za masomo kwa muda wa siku saba ili kupisha uchunguzi wa kina wa kubaini chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo.

Aidha, ameagiza Jeshi la Polisi, TAKUKURU, pamoja na wataalam wa ujenzi wa halmashauri kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na pia kukagua ubora wa majengo mengine shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema kuwa jana majira ya mchana walipokea majeruhi 31 wanafunzi 17 wa kiume na 14 wa kike. Hata hivyo, hakuna majeruhi aliye katika hali mbaya, na wote wanaendelea vizuri, hivyo muda wowote wanaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani.