Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea kumsaka dereva wa lori la kusafirisha mafuta, Abubakari Adam Mwichangwe, mkazi wa Dar es Salaam, kwa tuhuma za kula njama, kuharibu gari na kuiba mafuta lita 35,700 yenye thamani ya Shilingi milioni 77.11 mali ya kampuni ya ACER Logistics (T) Limited.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 18, 2025, na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 16, 2025. Dereva huyo alikuwa akiendesha lori lenye namba T.661 BXR likiwa limeunganishwa na tela namba T489 BHC aina ya Faw, mali ya kampuni ya Meru iliyopo Dar es Salaam. Lori hilo lilikuwa likisafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kuelekea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kamanda wa Polisi alieleza kuwa, akiwa njiani katika Mkoa wa Morogoro, dereva huyo alishirikiana na watu wengine katika mpango wa wizi wa mafuta hayo. Waliohusika ni pamoja na Hamidu Soud Hamidu (50), Meneja Mkuu wa kituo cha mafuta cha Simba Oil, mkazi wa Dar es Salaam; Abner Mwammar Shallom (25), Meneja wa kituo cha Simba Oil kilichopo Mkambarani, Morogoro; na Abdallah Nihed Abdallah (30), Meneja wa kituo cha Simba Oil kilichopo Morogoro Mjini. Mafuta hayo yaliibwa na kushushwa kwenye vituo vya mafuta vya kampuni hiyo.
Baada ya kuiba mafuta hayo, dereva aliendelea na safari akiwa na lori tupu. Alipofika katika eneo la Msufini, kijiji cha Msimba, barabara kuu ya Mikumi-Iringa, Wilaya ya Kipolisi Ruhembe (Kilosa), aliliingiza lori hilo korongoni kwa lengo la kuaminisha kuwa limepata ajali. Baada ya hilo, alijaribu kuliteketeza kwa moto ili kuficha ushahidi, lakini kabla moto haujasambaa, wananchi waliokuwa eneo hilo waliweza kuuzima na kutoa taarifa kwa polisi.
Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kumkamata dereva huyo huku uchunguzi zaidi ukiendelea kwa washirika wake waliokamatwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeeleza kuwa uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika. Aidha, jeshi hilo limetoa onyo kali kwa madereva na wahusika wa sekta ya usafirishaji kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali, kwani sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya kihalifu.
Leave a Reply