Dkt. Willibrod Slaa Arejea CHADEMA

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2010, Dk. Wilbroad Slaa, amerejea rasmi ndani ya chama hicho na kupokelewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Tundu Lissu katika uwanja wa Ruanda Nzovwe, Mbeya. Leo tarehe 23 Machi 2025 wakati Chama hicho kinazindua Operesheni #NoReformsNoElection katika jiji la Mbeya.

Dk. Slaa, ambaye alijiondoa katika siasa za Tanzania kwa muda mrefu, aliondoka Chadema mwaka 2015 kutokana na kutofautiana misimamo na viongozi wenzake, hasa baada ya chama hicho kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kama mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka huo.

Operesheni #NoReformsNoElection, ambayo ilizinduliwa rasmi leo jijini Mbeya, inalenga kushinikiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Chadema inataka mageuzi yanayohakikisha tume huru ya uchaguzi na uhuru wa vyombo vya habari katika mchakato wa kisiasa.

Kwa mujibu wa ratiba ya Chadema, operesheni hii itaendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, huku chama hicho kikihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kudai haki zao za kidemokrasia.