CCM Yatangaza kuanza Mchakato wa Uteuzi wa Wagombea kwa Uchaguzi Mkuu 2025

Chama Cha Mapinduzi CCM kimetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wake wa ndani wa kuwateua wagombea watakaokiwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho, mchakato utaanza rasmi Mei 1, 2025, kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi kwa nafasi za Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, na Udiwani. Zoezi hili litafanyika kwa muda wa siku kumi na tano, kuanzia saa 2:00 asubuhi ya Mei 1 hadi saa 10:00 jioni ya Mei 15, 2025.

Taarifa hiyo imeeleza kwa kina utaratibu ambao wanachama wanapaswa kufuata kulingana na nafasi wanayogombea:

Wanachama wanaowania Ubunge au Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watahitajika kuchukua na kurudisha fomu zao kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.

Kwa nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na makundi maalumu (NGOs, Wafanyakazi, Wasomi na Walemavu), wanachama watawasiliana na Katibu wa UWT wa Mkoa husika kwa ajili ya taratibu za fomu.

Wanachama wanaogombea Viti Maalumu vya wanawake (Bunge/Baraza la Wawakilishi) kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wataelekezwa kuchukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM Mkoa husika.

Utaratibu kama huo utafuatwa kwa wanachama wanaowania Viti Maalumu vya wanawake (Bunge/Baraza la Wawakilishi) kupitia Jumuiya ya Wazazi, ambapo watawasiliana na Katibu wa WAZAZI Mkoa husika.

Kwa ngazi ya Udiwani wa Kata (Bara) au Wadi (Zanzibar), wanachama watachukua na kurudisha fomu zao kwa Katibu wa CCM wa Kata/Wadi husika.

Wanachama wanaogombea Udiwani Viti Maalumu vya Wanawake watafanya taratibu zao za fomu kupitia Katibu wa UWT wa Wilaya husika.