Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa onyo kali kwa viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusiana na mipango yao ya kukusanyika katika eneo la Mahakama ya Kisutu tarehe 24 Aprili 2025
Katika taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Murilo, jeshi hilo limesema limekuwa likifuatilia matamko na mipango ya baadhi ya viongozi wa chama hicho, ambao wanadaiwa kuhamasisha watu kukusanyika siku hiyo wakati mmoja wa viongozi wao, Tundu Lissu, atakapofikishwa mahakamani.
Kamanda Murilo ameeleza kuwa jeshi la polisi lina taarifa za mipango ya CHADEMA kufanya vurugu kwa lengo la kushinikiza mamlaka za kisheria kumwachia mtuhumiwa huyo.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawakumbusha wahusika kuwa Mahakama ni Mamlaka za kisheria zilizo huru na hazipaswi kutishwa au kuingiliwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yake,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Aidha, jeshi la polisi limewataka wananchi wote wanaohamasishwa kuhusiana na nia hiyo “ovu” kutoshiriki kwenye mpango huo. Taarifa hiyo iliongeza kuwa onyo kali linatolewa kwa wale wote wanaopanga na ambao watajaribu kutekeleza kinachohamasishwa, kwani watashughulikiwa vikali sana lakini kwa mujibu wa sheria za nchi.
Leave a Reply