Sakata la mabinti wa Chuo kikuu, Mwijaku kuhojiwa na Polisi

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria kuhusu kuwahoji wahusika wa sakata la mabinti wanafunzi wa vyuo waliomdhalilisha binti mwenzao na kwamba Mwijaku, ambaye ametajwa katika sakata hilo atahojiwa pia.

Dkt. Gwajima ametoa taarifa hiyo kwa umma, kufuatia kuongezeka kwa maswali kutoka kwa wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya Mwijaku, ambaye jina lake limekuwa likitajwa mara kwa mara katika video zilizosambaa mitandaoni kuhusiana na tukio hilo.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hao, naye atahojiwa kwa mujibu wa Sheria,” amesema Dkt. Gwajima.

Aliongeza kuwa, baada ya mahojiano hayo, Wizara yake itaangalia mustakabali mzima wa maadili ya jamii na nafasi ya Mwijaku na wengine wote wenye nafasi zenye kuchochea kasi ya athari chanya au hasi kwenye maadili ya jamii.

Waziri Gwajima amewataka wananchi kuwa watulivu na kuendelea kufuatilia taarifa kutoka Jeshi la Polisi.