Tanzania yaondoa Marufuku ya uingizwaji wa Mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini

Serikali ya Tanzania imeondoa marufuku iliyokuwa imewekwa kwenye uingizaji wa mazao ya kilimo kutoka nchi za Malawi na Afrika Kusini, iliyotangazwa Aprili 23, 2025.

Marufuku hiyo ilitolewa awali kama hatua ya kujibu vizuizi ambavyo Tanzania iliwekwa na nchi hizo mbili kwa mazao yanayotoka Tanzania.

Baada ya zuio hilo, serikali za Malawi na Afrika Kusini zilifanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Kilimo za Tanzania kwa lengo la kutafuta suluhu ya pamoja.

Kuhusu Malawi, serikali imekubali kutuma ujumbe wa mawaziri tarehe 2 Mei 2025, utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, akifuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo. Ujumbe huu unatarajiwa kukutana na wenzao wa Tanzania jijini Dodoma kwa ajili ya mazungumzo yatakayoratibiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.

Kwa upande wa Afrika Kusini, mazungumzo ya kiufundi yanaendelea kati ya wataalam kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika za Afrika Kusini.

Wizara ya Kilimo imesema kuwa uamuzi wa kuondoa mazuio hayo kwa nchi zote mbili unatokana na imani kuwa mazungumzo yanayoendelea yatafikia suluhu yenye manufaa kwa pande zote.

Serikali imewatoa hofu wakulima na wananchi kwa ujumla, ikisisitiza kuwa inazingatia umuhimu wa biashara huria ya mazao ya kilimo, huku ikiweka kipaumbele kwenye afya ya mimea, rasilimali za taifa, na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kwa faida ya wote.