Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA John Edward Mrema, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zinazodai kuwa amevuliwa uanachama na tawi la Bonyokwa.
Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo, Bw. Mrema ameeleza kuwa taarifa hizo zimezua taharuki na kusababisha simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wanaotaka kujua ukweli, ambapo amebainisha mambo makuu matano yanayoonyesha kuwa barua inayosambaa haimuhusu yeye.
Mrema amesisitiza kuwa yeye ni mwanachama halali wa CHADEMA mwenye kadi namba 0111, na kwa mujibu wa kanuni za chama, wanachama wanatambulika kwa namba zao za kadi na kwamba Barua inayosambaa haikutaja namba yake, hivyo inaweza kumhusu mtu mwingine mwenye jina linalofanana.
Ameeleza kuwa CHADEMA ni chama cha kimtandao/kidigitali, na hata kadi yake ya uanachama haikutajwa kwenye barua hiyo, akionyesha uwezekano mkubwa kuwa taarifa hizo si za kweli, Bw. Mrema ameweka wazi kuwa yeye amesajiliwa katika tawi la Makongo, na si Bonyokwa kama inavyodaiwa. Ameongeza kuwa taarifa zake zote zinapatikana kwenye mfumo wa kidigitali wa chama
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa kanuni za chama (Kanuni ya 5.3), mwanachama anapaswa kuwasilisha taarifa zake kwa katibu wa tawi anapohama. Kwa kuwa hajawahi kufuata utaratibu huo kwa eneo la Bonyokwa, hajawahi kuwa mwanachama wa tawi hilo na hajawahi kushiriki vikao vyake.
Mrema amesisitiza kuwa tawi la Bonyokwa halina mamlaka ya kumvua uanachama kwa kuwa yeye si mwanachama wa tawi hilo. Ameongeza kuwa kadi yake inaonyesha tawi alilosajiliwa na taarifa zake zinapatikana kwenye mfumo rasmi wa CHADEMA Digital.
Mrema amesisitiza kuwa yeye ni mwanachama halali wa CHADEMA hadi pale hatua zitakapochukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama. Ameeleza kuwa Katiba ya chama (Ibara ya 5.4.3) inaeleza wazi taratibu na makosa yanayoweza kusababisha mwanachama kuvuliwa uanachama, ikiwemo kuwa na mwenendo usioendana na itikadi, falsafa, madhumuni, kanuni, maadili na sera za chama.
@Barakadon_
#WasafiDigital
John Mrema akanusha kuvuliwa uanachama CHADEMA

Leave a Reply