Urusi yaadhimisha siku ya Ushindi, Rais Samia atuma Barua ya Pongezi

Urusi imeadhimisha miaka 80 ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti  katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa kufanya gwaride kubwa la kijeshi katika Uwanja wa Red Square, jijini Moscow.

Maadhimisho hayo muhimu yameongozwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na kuhudhuriwa na zaidi ya viongozi 20 wa kimataifa, wakiwemo Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva, na Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuandikia barua ya pongezi Rais Putin kwa kuadhimisha Siku ya Ushindi.

“Kwa niaba ya Watanzania, nakutumia salamu za pongezi za dhati kwa kuadhimisha siku hii muhimu ambayo inaakisi historia ya kujitoa kwa ajili ya uhuru na haki,” ameandika Rais Samia.

Ameongeza kuwa kumbukumbu ya siku hiyo inaendelea kuzihamasisha nchi duniani kusimama kidete kulinda amani, haki na ushirikiano wa kimataifa.

Rais Samia pia amesisitiza kuwa Tanzania inathamini uhusiano wake na Urusi, uhusiano ambao umejengwa juu ya kuheshimiana na mshikamano. Amemtakia Rais Putin pamoja na wananchi wake mafanikio na ustawi endelevu.

Siku ya Ushindi huadhimishwa Mei 9 kila mwaka nchini Urusi kama kumbukumbu ya mwaka 1945 ambapo majeshi ya Umoja wa Kisovieti yalifanikiwa kuishinda Ujerumani ya Adolf Hitler na kufanikisha kumaliza Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

@barakadon_
#WasafiDigital