Tanzania na Zambia zakubaliana kuimarisha mpaka wa kimataifa

Tanzania na Zambia zimetiliana saini ya makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa mwishoni mwa wiki mara baada ya kukamilika kwa Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Zambia kilichofanyia kwa siku tano katika mji wa Tunduma mkoa wa Songwe.

Utiaji saini makubaliano hayo umefanywa kati ya kiongozi wa timu ya Tanzania ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansour na Bw. Kelvin Chibangula ambaye ni kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka nchini Zambia.

Akizungunza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo, mkuu wa timu ya Tanzania Bw. Hamdouny Mansour amesema, katika siku tano za kikao hicho wataalamu wameweza kupendekeza mawazo kwa utulivu, kuandaa bajeti pamoja na maazimio ya utekelezaji mpango wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo mbili.

Naye kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka nchini Zambia ambaye ni Mpima Mkuu Msaidizi Bw. Kelvin Chibangula ameeleza kuwa, kikao hicho ni ishara ya ujirani mwema na ushirikiano imara wa kidiplomasia unaoendelea baina ya Tanzania na Zambia.

Mpaka wa kimataifa wa Tanzania na Zambia una urefu wa takriban km 345 ambapo km 100 ni nchi kavu, km 189 ni mto Kalambo na km 56 ziwa Tanganyika.

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za afrika iwe imeimarishwa.