Kanisa la Askofu Gwajima Lafungiwa

Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel R. M. Kihampa, amefuta usajili wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima.

Katika Barua yake kwa Askofu Gwajima, Bw. Kihampa amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Askofu Gwajima kuonekana akitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa kupitia mimbari ya kanisa hilo, akielezwa kuwa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

“Vitendo hivi ni kinyume cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 chini ya kifungu cha 17, kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria namba 3 ya mwaka 2019, kwa kuwa vina athari ya kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,” amesema Kihampa.

Kwa mujibu wa barua hiyo, shughuli zote za kanisa hilo zinasitishwa mara moja kuanzia tarehe 2 Juni 2025, na usajili wake umefutwa rasmi kwa mamlaka ya kisheria aliyo nayo Msajili.

Hata hivyo, Msajili amebainisha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Jumuiya, kanisa hilo lina haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, ndani ya siku 21 tangu kutolewa kwa taarifa ya kufutwa kwa usajili.