NAIROBI, KENYA: Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya imetupilia mbali mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili mwanaharakati Boniface Mwangi. Uamuzi huu unakuja kufuatia siku kadhaa za sintofahamu kuhusu kesi yake.
Licha ya kufutwa kwa mashtaka ya ugaidi, Mwangi bado anakabiliwa na mashtaka mawili mengine: kumiliki silaha bila kibali na kupatikana na sumu pamoja na vitoa machozi. Alikanusha mashtaka hayo na ameachiliwa kwa bondi ya shilingi milioni moja za Kenya.
Kukamatwa kwa Boniface Mwangi kumelaaniwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu, ambayo yameeleza wasiwasi wao kuwa hatua hiyo inalenga kukandamiza sauti za upinzani nchini. Mwangi mwenyewe amekanusha vikali tuhuma hizo, akisisitiza kupitia chapisho kwenye mtandao wa X: “Mimi sio gaidi.”
Tuhuma zinazomkabili zinahusishwa na maandamano ya Juni 25, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) inayofadhiliwa na serikali. Maandamano hayo yalishuhudia mapigano kati ya waandamanaji na polisi, na kusababisha vifo vya watu 19, mamia ya majeruhi, na uharibifu wa mali.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, ameelezea maandamano hayo kama “ugaidi uliojificha kama upinzini” na “jaribio lisilo la kikatiba” la kuiangusha serikali. KNCHR pia imeripoti kuwa watu wengine 38 waliuawa katika maandamano yaliyofuata mapema mwezi huu. Tangu Juni mwaka jana, zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha katika wimbi la maandamano ya kupinga serikali, huku polisi wakituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Leave a Reply