Mke mkubwa awachinja watoto watatu wa Mke mdogo

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia Wende Luchagula, Miaka 30, Kabila Msukuma, Mkazi wa Kijiji cha Milonji kwa kosa la mauaji baada ya kuwachinja watoto wa mke mwenzake watatu mpaka kufa.

Tukio hilo limetokea Julai 12, 2025 majira ya saa nane mchana huko Kijiji cha Milonji, Kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo ambapo mtuhumiwa alivizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao ambaye ni mke mdogo wakiwa wameenda mnadani kisha akatekeleza tukio hilo la kuwachinja watoto watatu kati yao wawili wakiwa mapacha ambao ni Lugola Lutelemula Samweli (6), Kulwa Lutelemula Samweli, Umri miezi 8 na Doto Lutelemula Samweli Umri Miezi 8, wote wakazi wa Kijiji cha Milonji chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi.

Akizungumza na vyombo vya habari kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma SACP- Marco Chilya amesema, mume wa mtuhumiwa huyo alikuwa ameoa wake watatu lakini alikuwa akimpenda zaidi mke mdogo na Watoto wake kitendo ambacho mtuhumiwa hakukipenda ndipo akavizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao ambaye ni mke mdogo wakiwa wameenda mnadani kisha akatekeleza tukio hilo la kikatili la kuwa chinja watoto hao mpaka kufa.

Miili ya marehemu imekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi. Mtuhumiwa amekamatwa kwa hatua zaidi za kisheria.