Rais Samia kuzindua bandari kavu ya Kwala Julai 31

Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inatarajia kuzindua Bandari kavu ya Kwala,  safari za treni ya mizigo ya SGR kati ya Dar es Salaam – Dodoma, pamoja na Upokeaji wa mabehewa mapya 50 ya mizigo ya Treni ya Kawaida (MGR) .

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesema Moja ya changamoto kubwa zilizokuwa zikiikabili Bandari ya Dar es Salaam kuanzia miaka ya 2008 ni msongamano wa meli unaotokana na mrundikano mkubwa wa Shehena na hivyo Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Bandari Kavu (Inland Container Depots – ICDs) katika maeneo mbalimbali nchini.

“Bandari kavu ya Kwala inatarajiwa kuhudumia shehena ya makasha yanayokwenda nchi jirani na itakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku, hivyo kuifanya Bandari hiyo kuhudumia hadi makasha 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa” amesema Waziri Mbarawa.

Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo utakaofanyika Julai 31 mwaka huu wa 2025 katika eneo la Kwala Wilaya ya Kibaka Mkoani Pwani anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.