Chama cha ACT Wazalendo kimetoa Taarifa kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, leo imetoa agizo kwa Serikali, ikiipatia muda wa siku tano (5) kujibu kesi iliyofunguliwa na Chama cha ACT Wazalendo na Bw. Luhaga Joelson Mpina.
Kesi hiyo inahusu madai ya ukiukwaji wa Katiba na Sheria za Uchaguzi wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais uliokamilika Agosti 27, 2025. huku lmbi la upande wa Serikali la kuongezewa siku 14 kwa ajili ya kuwasilisha majibu likikataliwa.
Taarifa ya ACT imeeleza Mahakama imetamka kuwa, licha ya zoezi la uteuzi kumalizika jana tarehe 27 August 2025, endapo itajiridhisha kuwa Tume ya Uchaguzi ilikiuka Katiba, Sheria na Kanuni katika kumzuia Ndugu Luhaga Joelson Mpina kurejesha fomu, haitasita kutoa amri ya kumpa fursa ya kurejesha fomu na kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kuzingatia kuwa shauri hili lina maslahi mapana ya kitaifa na umma, Mahakama imetoa maagizo kwamba kesi itatajwa na kuanza kusikilizwa kwa njia ya mtandao tarehe 3 Septemba 2025, saa 3:00 asubuhi. Wananchi wote wamekaribishwa kufuatilia mwenendo wa kesi kupitia kiunganishi (link) kitakachotolewa na Mahakama.” – imeeleza Taarifa ya ACT Wazalendo
Leave a Reply