Katika hatua kubwa ya kihistoria kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), dawa mpya ya kudungwa inayoitwa Lenacapavir inatarajiwa kupatikana kwa gharama nafuu katika nchi 120 zenye kipato cha chini na cha kati kuanzia mwaka 2027.
Dawa hiyo itauzwa kwa kiasi cha dola 40 pekee kwa mwaka, sawa na gharama ya vidonge vya kila siku vya kujikinga na VVU (PrEP), hatua inayotarajiwa kuongeza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa kinga dhidi ya maambukizi mapya ya virusi hivyo.
Makubaliano ya kuruhusu uzalishaji na usambazaji wa dawa hiyo kwa bei nafuu yamesimamiwa na mashirika ya kimataifa likiwemo UNITAID, ambalo ni shirika tanzu la Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na Mpango wa Afya wa Clinton (CHAI), Wits RHI na Maabara ya Dkt. Reddy.
Lenacapavir, inayodungwa mara mbili tu kwa mwaka, imeonesha ufanisi mkubwa katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU na inachukuliwa kama suluhisho muhimu kwa watu wanaopata changamoto za kutumia dawa za kila siku kama PrEP.
Tafiti zimeonesha kuwa dawa hiyo hufanya kazi kwa kuzuia virusi vya VVU kujizalisha ndani ya seli za mwili, na hivyo kutoa kinga ya muda mrefu dhidi ya maambukizi. Dawa hiyo tayari imeidhinishwa na Shirika la Chakula na Dawa la Marekani (FDA) na Tume ya Ulaya, huku WHO ikipendekeza matumizi yake kama njia bora ya kuzuia maambukizi mapya.
Wataalamu wa afya wanasema hatua hii itasaidia kuongeza kasi ya kupunguza maambukizi mapya, hasa katika makundi yaliyo kwenye hatari kubwa kama vijana, wanawake na watu wanaotumia dawa za kulevya
Kwa mujibu wa UNAIDS, zaidi ya watu milioni 40 duniani wanaishi na VVU, huku takribani milioni 1.3 wakiambukizwa mwaka uliopita. Upatikanaji wa dawa hii kwa bei nafuu unatarajiwa kuwa hatua muhimu kuelekea kumaliza janga la UKIMWI duniani.
Leave a Reply