Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, amesema hatastaafu kucheza soka hadi atakapofanikisha lengo lake la kufunga mabao 1,000 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 40, alitoa kauli hiyo baada ya kutajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashariki ya Kati katika Tuzo za Soka za Globe zilizofanyika Dubai. Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya mshambuliaji huyo kufunga mabao mawili katika ushindi wa Al-Nassr wa 3–0 dhidi ya Al Akhdoud, na kufikisha jumla ya mabao 956 aliyofunga katika maisha yake ya soka.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Ronaldo alisema bado ana motisha na shauku kubwa ya kuendelea kucheza soka licha ya umri wake, akisisitiza kuwa anafurahia mchezo huo popote anapocheza.
“Ni vigumu kuendelea kucheza, lakini nina motisha. Shauku yangu ni kubwa na ninataka kuendelea. Lengo langu ni kufunga mabao 1,000 na nitalifikia kama sitapata majeraha,” alisema Ronaldo.
Mshambuliaji huyo alijiunga na klabu ya Al-Nassr mwaka 2022 na Julai mwaka huu alisaini mkataba mpya wa miaka miwili unaomuweka klabuni hapo hadi atakapovuka umri wa miaka 42.
Katika msimu wa sasa wa Ligi ya Saudi Pro, Ronaldo amefunga mabao 13 katika mechi 14, huku Al-Nassr wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na faida ya pointi nne dhidi ya wapinzani wao wa karibu.
Ronaldo anashikilia rekodi kadhaa muhimu, zikiwemo kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ureno (mabao 143) na Real Madrid (mabao 450). Pia ndiye mchezaji pekee aliyefunga zaidi ya mabao 100 akiwa na vilabu vinne tofauti: Manchester United, Real Madrid, Juventus na Al-Nassr.
Aidha, Ronaldo amethibitisha kuwa Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico litakuwa mashindano yake ya mwisho katika ngazi ya kimataifa. Aliwahi kuiongoza Ureno kushinda Euro 2016 nchini Ufaransa, mafanikio makubwa zaidi katika historia ya soka ya taifa hilo.









Leave a Reply