Trump: kuna maendeleo katika mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine

Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamesema kuwa kuna maendeleo makubwa yamepatikana katika mazungumzo yanayolenga kumaliza vita vya Ukraine, ingawa suala la mpaka wa Donbas bado halijapatiwa suluhu ya mwisho.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makazi ya Rais Trump ya Mar-a-Lago huko Florida, Rais Zelensky alisema pande hizo mbili zimekubaliana takribani asilimia 90 ya mpango wa amani unaojumuisha vipengele 20. Kwa upande wake, Rais Trump alisema kuwa makubaliano kuhusu dhamana ya usalama kwa Ukraine yamekamilika kwa karibu asilimia 95.

Hata hivyo, Trump alikiri kuwa pendekezo la kuifanya eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine kuwa eneo lisilo la kijeshi bado halijatatuliwa, likibaki kuwa mojawapo ya changamoto kuu katika mazungumzo hayo.

Baadaye, Rais Zelensky alitangaza kuwa timu za Marekani na Ukraine zinatarajiwa kukutana tena wiki ijayo kwa mazungumzo ya kina zaidi yanayolenga kukomesha vita vinavyoendelea dhidi ya Urusi.

“Tulikuwa na mazungumzo muhimu kuhusu masuala yote na tunathamini maendeleo ambayo timu za Ukraine na Marekani zimepiga katika wiki zilizopita,” Zelensky alisema kupitia taarifa aliyotoa kwenye mtandao wa Telegram.

Kwa mujibu wa taarifa, Urusi kwa sasa inadhibiti takribani asilimia 75 ya mkoa wa Donetsk na karibu asilimia 99 ya mkoa wa Luhansk. Mikoa hiyo miwili kwa pamoja inajulikana kama Donbas.

Urusi inasisitiza kuwa Ukraine inapaswa kujiondoa katika maeneo ya Donbas ambayo bado iko chini ya udhibiti wa Kyiv, huku Ukraine ikipendekeza eneo hilo liwe eneo huru la kiuchumi linalolindwa na vikosi vya Ukraine.

Urusi ilianzisha uvamizi wake dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022, na kwa sasa inadhibiti takribani asilimia 20 ya eneo lote la Ukraine. Vita hivyo vimeingia karibu mwaka wake wa nne, vikiendelea kuathiri usalama wa kikanda na wa kimataifa.

Mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Ukraine yanaonekana kutoa mwanga wa matumaini, ingawa masuala nyeti ya mipaka na udhibiti wa maeneo bado yanahitaji maridhiano ya kina.