Dugange Aitaka NEMC ‘Kukaza Uzi’ Usimamizi wa Mazingira

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.Dkt. Festo Dugange, amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha linasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira katika miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Kagera, ili kulinda rasilimali za mazingira na afya za wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya mazingira katika Halmashauri za Wilaya ya Karagwe na Misenyi, Dkt. Dugange alisisitiza kuwa NEMC inapaswa kuimarisha ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi, kuhakikisha tathmini za athari kwa mazingira (EIA) zinafanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba masharti yote ya kimazingira yanazingatiwa kabla na wakati wa utekelezaji.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alikagua mradi wa vijana wa kuchakata taka za plastiki unaosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kutoa ajira kwa vijana. Pia alitembelea mradi wa biashara ya kaboni kupitia kilimo mseto (Kinoni Agroforestry Farm) unaotekelezwa na kampuni ya KADERES, unaolenga kuwawezesha wakulima kunufaika na biashara ya hewa ukaa sambamba na kuhifadhi mazingira.

Aidha, alikagua Kiwanda cha Vifungashio (Magunia) cha KADERES, Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia unaohamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza ukataji miti, pamoja na mradi wa ujenzi wa dampo la kuhifadhia maji taka wilayani Karagwe unaolenga kuboresha usafi wa mazingira na kulinda afya ya jamii.

Akizungumza na wananchi wa Karagwe na Misenyi, Dkt. Dugange alihamasisha jamii kuona mazingira kama fursa ya kiuchumi. Alieleza kuwa taka zinaweza kuwa rasilimali yenye thamani endapo zitasimamiwa na kuchakatwa kwa usahihi.

“Taka si taka tu bali ni rasilimali muhimu inayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi. Taka zinazooza zinaweza kutumika kutengeneza gesi na mbolea ya asili kwa ajili ya bustani za kioganiki na kulinda rutuba ya udongo,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja NEMC Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Bw. Boniphace Guni, amesema NEMC itaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi yote inayotekelezwa katika kanda hiyo na kuhakikisha sheria za mazingira zinatekelezwa kikamilifu nchini kote.

Ziara hiyo pia ilihusisha ushiriki wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha maendeleo endelevu yanakwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.