Ajali ya Treni Yaathiri Abiria 10 Jijini Dar es Salaam

Treni ya abiria ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) inayotoa huduma ya usafiri wa mjini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu, imepata ajali leo jioni katika makutano ya reli na barabara ya Kawawa, saa chache baada ya kuanza safari.

Ajali hiyo imetokea saa 10:05 jioni, dakika chache baada ya treni hiyo kuondoka stesheni ya Kamata. Treni hiyo ilikuwa imebeba takribani abiria 1,200 katika mabehewa 12.

Timu ya wataalamu wa TRC pamoja na kikosi cha huduma za afya cha shirika hilo walifika haraka eneo la tukio na kutoa msaada wa huduma ya kwanza kwa majeruhi. Jumla ya watu 10, wakiwemo wanaume wawili na wanawake wanane, wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa matibabu zaidi.

Ajali hiyo imesababisha mabehewa sita kuathirika, huku chanzo chake kikiwa hakijafahamika hadi sasa. TRC imeeleza kuwa uchunguzi unaendelea na taarifa zaidi zitatolewa kadri hali itakavyoruhusu.

Licha ya tukio hilo, Shirika la Reli Tanzania limeuarifu umma kuwa huduma ya usafiri wa treni ya mjini kuelekea Pugu itaendelea kama kawaida kuanzia kesho.

TRC imeeleza kuwa inaungana na wote walioathiriwa na ajali hiyo na linaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya majeruhi na maendeleo ya uchunguzi wa ajali hiyo.