Malengo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa kituo kikuu (hub) cha kuhudumia shehena ya mizigo inayokwenda nchi jirani, yameanza kuzaa matunda, baada ya bandari hiyo kuanza kupokea meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 300.
Mafanikio haya yametokana na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia mradi wa maboresho wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP).
Kwa mara nyingine katika historia yake, Bandari ya Dar es Salaam imefanikiwa kuhudumia meli kubwa ya Mv. MYNY aina ya Post Panamax, yenye urefu wa mita 300, uwezo wa kubeba tani 75,201 ikiwa imebeba shehena ya makasha 6,840.
Akizungumza mara baada ya meli hiyo kufunga gatini, Mkurugenzi wa Marini na Shughuli za Kibandari, Kapteni Abdallah Y. Mwingamno, amesema hatua hiyo ni ushahidi wa uwezo mpya wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa za kizazi cha sasa.
“Mafanikio haya ni matokeo ya maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali kupitia TPA. Tunapenda kuwahakikishia wateja na wadau wetu kwamba sasa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa na za kisasa kwa ufanisi zaidi,” alisema Kapteni Mwingamno.
Ameeleza pia kuwa mbali na maboresho ya miundombinu, Serikali kupitia TPA imewekeza kwenye ununuzi wa mitambo ya kisasa ikiwemo Ship to Shore Gantry Cranes (STS), Rubber Tyred Gantry Cranes (RTG), Reach Stackers na Forklifts za kisasa, ambayo itapunguza muda wa meli kukaa bandarini kwa kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji mizigo.
Katika maboresho hayo, kupitia Mradi wa DMGP, Serikali imeimarisha gati namba 1–7 kwa kuongeza kina kutoka mita 8 hadi mita 14.5, sambamba na kuongeza eneo la kuhudumia mizigo. Aidha, eneo la kugeuzia meli (turning basin) limeongezwa kina hadi mita 15 ili kuruhusu meli kubwa zaidi kuhudumiwa kwa ufanisi.
Vilevile, lango la kuingilia meli limepanuliwa na kuongeza kina chake ili kuruhusu meli zenye upana mkubwa kuingia bila changamoto.
Mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unagharimu Shilingi trilioni 1.118, ambazo zinatokana na mkopo wa Benki ya Dunia, misaada ya wafadhili na mapato ya ndani ya TPA. Mradi huu umehusisha pia ujenzi wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari (RoRo Berth), kuimarisha gati za 8–11 kwa kuongeza kina kutoka mita 12 hadi mita 14.5, kuboresha mtandao wa reli ndani ya bandari na usimikaji wa mfumo wa umeme bandarini.
Kwa maboresho haya, Bandari ya Dar es Salaam sasa imejiweka kwenye nafasi ya ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji mizigo.
Leave a Reply