Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesema dhana inayodai kuwa chai ya Tanzania haitumiki au hainyweki katika soko la dunia si ya kweli bali ni uongo usio na msingi wowote.
Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa wadau wa tasnia ya chai nchini, Mhe. Bashe alifafanua kuwa serikali imefanya uchunguzi wa kina juu ya mwenendo wa chai ya Tanzania katika masoko ya kimataifa, na kubaini kuwa bidhaa hiyo inahitajika sana endapo itazalishwa kwa ubora unaokubalika.
“Watu wanahitaji chai ya Tanzania lakini si makapi. Wanahitaji chai bora,” alisema Mhe. Bashe. Aliongeza kuwa kwa kuwatuma watu wake kufanya utafiti, amepata ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa soko la kimataifa linapokea vizuri chai ya Tanzania inayozingatia viwango vya ubora.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe alitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Bi. Beatrice Banzi, na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Abdulmajid Nsekela, pamoja na wadau wengine wa tasnia hiyo, kuacha mara moja kuendeleza hoja ya kwamba chai ya Tanzania hainyweki duniani.
“Msirudi tena kwangu na hoja hiyo. Utafiti tuliofanya una mashiko, na ukweli ni kwamba bidhaa yetu inapendwa nje ya nchi – tunachotakiwa ni kuboresha ubora na ufanisi katika mnyororo mzima wa thamani,” alisisitiza.
Tasnia ya chai ni miongoni mwa sekta muhimu za kilimo zinazochangia pato la taifa na ajira kwa maelfu ya Watanzania, hususan katika maeneo ya nyanda za juu kusini na kaskazini mwa nchi.
Leave a Reply