Mkurugenzi wa Wasafi, Naseeb Abdul Juma (Diamond Platnumz), amezindua rasmi bidhaa mpya ya sabuni iitwayo Wasafi Soap, katika hafla ya Wasafi Iftar iliyofanyika leo katika ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wadau wa sanaa pamoja na wafanyabiashara mbalimbali
Akizungumza katika hafla hiyo, Diamond Platnumz alisema kuwa uzinduzi wa Wasafi Soap ni sehemu ya juhudi zake za kupanua uwekezaji katika sekta ya biashara na viwanda nchini, huku akisisitiza dhamira yake ya kuleta bidhaa bora sokoni.
Diamond , ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Kupitia ujumbe wake, Diamond Platnumz pia ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya Waziri Selemani Jafo, akisema kuwa ufanisi katika sekta hiyo umeongezeka kwa kiasi kikubwa

“Ningependa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia Wizara ya Viwanda na Biashara chini yako Waziri Jafo, hakika ufanisi umeongezeka,” amesema Diamond Platnumz.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amepongeza juhudi za Wasafi katika kuwekeza katika sekta ya viwanda, akisema kuwa hatua hiyo inasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa vijana.
Wasafi Soap ni kielelezo cha maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati, ambavyo vinasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hafla ya Wasafi Iftar ni miongoni mwa matukio muhimu yanayoandaliwa kila mwaka na Wasafi, kwa lengo la kuungana na jamii katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.



Leave a Reply