Jaji Mkuu afungua mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji , Naibu wasajili, Mahakimu

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju amefungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji, Naibu Wasajili na Mahakimu na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia haki na uadilifu katika utendaji wa kazi.

Mhe. Masaju amefungua mafunzo hayo leo Agosti 28 katika ukumbi uliopo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yatafanyika kwa makundi mbali mbali mpaka Septemba 19, 2025.

Jaji Mkuu amesema kuwa kazi ya utoaji maamuzi ni kubwa sana kwani inatambulika hata katika vitabu vya dini na hivyo kuwasisitiza washiriki wa mafunzo kufahamu kuwa wana jukumu zito ambalo wanapaswa kulipa umuhimu mkubwa.

Awali, Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya tatu na ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ambapo moja ya eneo unagusia suala la kujengeana uwezo katika utendaji wa kazi wa kila siku.

Pia ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya Mpango Mkakati wa IJA nani Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani amesema: “Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi unakuwa wa haki.”

Vilvile ameongeza kuwa ana imani mafunzo hayo yataimarisha weledi, uwajibikaji na maadili kwa washiriki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu nane ambazo zitajumuisha Majaji Wafawidhi na baadhi ya Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa na Wilaya, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Ni utamaduni wa Mahakama kutayarisha mafunzo kama haya kabla ya kila Uchaguzi Mkuu. Lengo kuu ni kuwaweka tayari Maafisa wa Mahakama ambao wanaweza kupangiwa majukumu ya kusikiliza mashauri ya uchaguzi ili waweze kuyaendesha kwa weledi, kwa wakati, kwa uwazi na haki.