Jela miaka 30 kwa kumbaka mtoto wake wa kumzaa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Lindi, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Alli Ibrahimu Malinda (30), mkazi wa Kijiji cha Ng’apa, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 10. Hukumu hiyo imetolewa Julai 23, 2025 na Hakimu Mkazi Delphina Kimathi, baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo shaka yoyote.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, tukio hilo lilitokea Januari 6, 2025, usiku katika kijiji cha Ng’apa, wakati mtoto huyo akiwa usingizini. Malinda alitumia nafasi yake kama mzazi vibaya na kutenda kitendo hicho cha unyama ndani ya nyumba yao ya familia.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kimathi alisema kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha wazi kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo la ukatili wa kingono dhidi ya mtoto wake, na kwamba mahakama haiwezi kuvumilia matendo kama hayo yanayohatarisha ustawi na haki za watoto.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Denis Nguvu, uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo. Katika uamuzi wake, mahakama ilisema adhabu hiyo ni sahihi kwa kuzingatia uzito wa kosa na madhara aliyoyapata mtoto huyo