Mahakama ya Wilaya ya Geita imemhukumu Rehema John (24) kifungo cha miaka mitano jela, faini ya Sh milioni 1 na fidia ya Sh milioni 2 kwa kosa la kummwagia chai ya moto mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba na kumsababishia majeraha makubwa.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Bruno Bongole, katika Kesi ya Jinai Na. 0495/2025, ambapo mshtakiwa alipatikana na hatia kwa mujibu wa Kifungu cha 169A (1) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Godfrey Odupoy akisaidiana na Wakili Consesa Desideri, tukio hilo lilitokea Agosti 3, 2024 majira ya saa 3:00 asubuhi katika Mtaa wa Mwembeni, Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita.
Imeelezwa kuwa mshtakiwa alimmwagia chai ya moto mtoto huyo aliyekuwa chini ya uangalizi wake, kitendo kilichomsababishia maumivu makali na majeraha kwenye mguu wa kushoto.
Ushahidi wa mashahidi watano uliotolewa na upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka, na Mahakama ikaona mshtakiwa ana hatia.
Katika utetezi wake, Rehema aliomba apewe adhabu ndogo kwa maelezo kuwa ana mtoto mchanga wa miezi minne.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba mnipunguzie adhabu kwa kuwa nina mtoto mchanga,” alieleza Rehema mbele ya Mahakama.
Hata hivyo, Hakimu Bongole alisema Mahakama imezingatia pia Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Mtoto (Sura ya 13, marejeo ya 2019) na kuona ni muhimu kutoa adhabu hiyo kama fundisho kwa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto
Leave a Reply