Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga yatembea kifua Mbele usikilizaji wa Mashauri



Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga inayojumuisha mikoa ya Shinyanga na Simiyu inatarajia kufanya maadhimisho ya wiki ya sheria yenye lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi Januari 25, 2025 mkoani Shinyanga.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 20, 2025 Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga Jaji Frank Mahimbali amesema  kuelekea wiki na siku ya sheria nchini inayoongozwa na kauli isemayo ‘Tanzania 2050 Nafasi ya Taasisi  zinasimamia Haki Madai katika Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’ amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuweza  kujua mambo mbalimbali yanayohusu sheria.

Jaji Mahimbali amebainisha  Mafanikio ya utendaji kazi wa shughuli za mahakama kwa kanda ya Shinyanga ambapo amesema Mahakama ilijikita kuhakikisha utoaji wa haki unafanyika kwa wakati na kwa watu wote  kwa kufanya uboreshaji wa utendaji kazi wa Mahakama Kidigital na kueleza hatua zilizofikiwa katika usikilizaji wa mashauri kwenye mahakama za kanda ya Shinyanga.

Ameongeza kuwa kauli mbiu hiyo inawasaidia kutumia mkakati na ufanyaji wa maboresho ya Mahakama hasa wanapoiendea dira mpya ya matumaini ya mafanikio 2050, ya uchumi wa kiwango cha kati ngazi ya juu, na wamejipanga kufanikisha mpango huo na watakuwa watekelezaji wakubwa wa Dira hiyo ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050.

Nao baadhi ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga wametoa maoni yao kuelekea wiki ya sheria nchini na kueleza namna utolewaji wa elimu ya masuala ya sheria kwa wananchi unavyosaidia kupunguza migogoro kwenye jamii.