Moto waua watu 16 katika nyumba ya wazee

Watu kumi na sita wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia moto ulioteketeza nyumba ya wazee katika jiji la Manado, mji mkuu wa jimbo la Sulawesi Kaskazini, kaskazini mwa Indonesia, maafisa wa serikali ya mtaa wamesema.

Kwa mujibu wa idara ya zimamoto, taarifa za moto katika Nyumba ya Wazee ya Damai zilipokelewa Jumapili usiku, ambapo vikosi vya uokoaji vilifika eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima moto huo usiku huo huo.

Mkuu wa zimamoto na uokoaji wa jiji la Manado, Jimmy Rotinsulu, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wengi wa waliopoteza maisha walikutwa ndani ya vyumba vyao, hali inayoashiria kuwa huenda walishindwa kujinusuru wakati moto ulipozuka.

Polisi wamesema bado wanaendelea kuchunguza chanzo cha moto, huku juhudi za kuwatambua marehemu zikiendelea. Familia za waathirika zimeombwa kuwasiliana na hospitali ambako miili ya marehemu imehifadhiwa.

Afisa mmoja wa eneo hilo alikiambia chombo cha habari cha mtandaoni cha Detikcom kuwa miili mingi ipo katika hali isiyotambulika, jambo linaloifanya kazi ya utambuzi kuwa ngumu.

Tukio hili linajiri wakati ambapo masuala ya usalama wa majengo yanaendelea kuibua wasiwasi nchini Indonesia. Mapema mwezi huu, moto mwingine katika jengo la ghorofa saba jijini Jakarta uliua watu 22, tukio lililozua mjadala mpana kuhusu viwango vya usalama wa moto nchini humo.

Uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha mkasa huo na iwapo kulikuwa na uzembe wowote uliochangia kutokea kwa janga hilo.