Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa tuzo na vyeti kwa Shule za Ssingi zinazofanya vizuri kwenye uhifadhi wa mazingira katika Mkoa wa Dar es Salaam, wakati wa sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Kimkoa Juni 5, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira ili kuunga mkono maendeleo endelevu ya Taifa. “Tunahitaji kuongeza juhudi za pamoja katika kulinda mazingira yetu, kwani mafanikio ya Dira 2050 yanategemea namna tunavyohifadhi rasilimali za mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Kaimu Meneja wa Kanda ya Ilala, Bi. Zainab Kuhanwa, ametoa salamu za Baraza Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, na kuongeza kuwa NEMC kwa kushirikiana na KPMG Advisory Limited iliandaa mashindano ya shule za msingi ili kutambua na kuthamini juhudi za uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuhamasisha wanafunzi kuwa mabalozi wa mazingira katika jamii.

Ameeleza kuwa shule washindi zilipatikana baada ya tathmini iliyozingatia vigezo mbalimbali vya usimamizi wa mazingira ikiwemo uwepo wa Klabu za Mazingira, upandaji wa miti, usimamizi wa taka na usafi wa mazingira. Amesema utoaji wa tuzo na vyeti hivyo unalenga kuhamasisha Shule na Wadau wengine kuendelea kushiriki katika kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.







Leave a Reply