Padri Charles Kitima ashambuliwa, Polisi wamshikilia mmoja kwa mahojiano

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia na kumhoji mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam, Rauli Mahabi, kwa tuhuma za kuhusika katika shambulio dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima. Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo, Alhamisi, Mei 1, 2025, katika eneo la Baraza la Maaskofu, Kurasini, Temeke, jijini Dar es Salaam.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa Padri Kitima alikuwa amehudhuria kikao na viongozi wa dini mbalimbali kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni. Baada ya kikao hicho, alikwenda kwenye kantini ya eneo hilo ambako alikaa hadi saa nne na robo usiku. Inadaiwa kuwa alipokuwa akielekea maliwatoni pembeni ya kantini hiyo, alishambuliwa kichwani na watu wawili kwa kutumia kitu butu.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia na kumhoji Mahabi kuhusiana na tukio hilo.

“Anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo. Uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na za haraka zichukuliwe kwa wahusika,” alieleza Kamanda Muliro.

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi imefafanua kuwa Padri Kitima alipelekwa haraka katika Hospitali ya Aga Khan ambako anaendelea kupokea matibabu na hali yake kwa sasa inaelezwa kuwa inaendelea vizuri.

Kamanda Muliro amesema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini mazingira kamili ya tukio na kuwafikisha wahusika wote kwenye vyombo vya sheria.