Papa Francis ameruhusiwa kutoka hospitali ya Roma

Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, ameruhusiwa kuondoka katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma baada ya kulazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja. Kabla ya kuondoka, alijitokeza kwenye dirisha la hospitali hiyo Jumapili na kutoa baraka kwa waumini kwa mara ya kwanza tangu alazwe tarehe 14 Februari.

Kwa mujibu wa madaktari, Papa alipitia vipindi viwili muhimu ambapo maisha yake yalikuwa hatarini. Hata hivyo, Dk. Sergio Alfieri, mmoja wa madaktari wake, amethibitisha kuwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki hana tena nimonia.

Ingawa hajapona kabisa, Papa Francis anatarajiwa kupumzika kwa angalau miezi miwili huko Vatican kabla ya kurejea kikamilifu katika majukumu yake ya kichungaji. Madaktari wanasema atarejea kazini haraka iwezekanavyo ikiwa hali yake itaendelea kuimarika.