Rais Samia akoshwa na Ushirika, “nilikuwa naona kama ushirika ni chaka la wizi”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa yeye ni miongoni mwa wale waliokuwa hawana imani na vyama vya ushirika, akiviona kama maeneo ya wizi na udanganyifu. Hata hivyo, amebainisha kuwa mabadiliko yaliyofanyika yamefanya ushirika kusimama imara na kumfanya ahisi hamu ya kuendelea kuusaidia.

Akizungumza leo, Aprili 28, 2025, wakati wa uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank) jijini Dodoma, Rais Samia alisema, “Wale ambao walikuwa hawana imani sana na ushirika, mimi nilikuwa mmoja wapo, sio Bashe peke yake. Nilikuwa naona kama ushirika ni chaka la wizi, na nadhani siku nilipozungumza nanyi Ikulu nilisema hivyo: ‘nendeni mkabadilike, ushirika mna sifa mbaya.’ Lakini jinsi tunavyokwenda, viongozi wapya kuingia, mifumo kubadilishwa, hili kubadilishwa, ushirika sasa umesimama vizuri, umesimama vizuri kiasi ambacho unazidi kunipa hamu nifanye zaidi kusaidia maendeleo ya ushirika nchini.”

Rais Samia aliwataka viongozi wanaohusika na ushirika, Tume ya Ushirika, na wadau wengine, kuhakikisha wanasimamia ushirika ili uwe imara zaidi. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea na mabadiliko chanya ili kuimarisha sekta hiyo na kuleta manufaa kwa wanachama.