Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuongeza vyumba vya upasuaji katika Taasisi ya Moyo na Mifupa (MOI) ili kuongeza kasi ya utoaji wa huduma hizo kwa watu wengi zaidi kwa kuwa kumekua na ongezeko la magonjwa hayo yanayotokana na ajali.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo Juni 09, 2025 wakati akizindua bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo na Mifupa (MOI) katika ofisi za Wizara ya Afya Mkoani Dodoma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Martina Njelekela.
“Tutashirikiana kuongeza vyumba vya upasuaji vingi kadiri inavyowezekana ili upasuaji uweze kufanyika usiku na mchana kwa kutoa huduma kwa watu wengi na kwa wakati kwa kuwa magonjwa haya yanatokana na ajali, na mtu akipata ajali anatakiwa kuhudumiwa haraka,” amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ameitaka bodi hiyo kusimamia kwa ufanisi ubora wa huduma, kuimarisha huduma kwa wateja, kukuza tiba utalii, kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuanzisha huduma mpya za kibobezi, kuongeza uwajibikaji wa matokeo na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kitaaluma.
“Uteuzi wa bodi hii mpya una lengo la kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo muhimu na kuhakikisha MOI inaendelea kuwa kinara wa utoaji wa huduma bora za kibingwa na kibobezi katika eneo la mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu,” amesema Waziri Mhagama
Pia, Waziri Mhagama amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia imewekeza zaidi katika Sekta ya Afya kwa kuanzisha huduma mpya katika taaisisi ya MOI ikiwemo kuanzishwa kwa huduma mpya ambazo hazikuwepo awali nchini ikiwemo, upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili bandia, upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu madogo.
“Upasuaji wa ubongo kwa kutumia mawimbi ya sauti, kunyoosha vibiongo kwa watoto, upasuaji wa magoti na mabega kwa teknolojia ya matundu, upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu, upasuaji wa marudio wa nyonga na magoti pamoja na upasuaji wa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo,” amesema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya wadhamini ya MOI Dkt. Martina Njelekela amesema wamepokea kwa moyo mkunjufu na kuahidi kuyatekeleza maelekezo yote waliyopatiwa na Mhe. Waziri ikiwa ni utekelezaji pia wa maelekezo ya Rais.
Leave a Reply