Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekabidhiwa rasmi umiliki wa timu ya Tabora United na kuibadilisha jina kuwa TRA United Sports Club.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA, timu hiyo ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu Tanzania sasa itakuwa mali ya walipakodi na Watanzania wote, na itaendelea kuwepo katika Mkoa wa Tabora.
Mbali na kushiriki katika mashindano ya soka na kutoa burudani kwa wananchi, TRA United Sports Club itakuwa na malengo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari, kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi, kuendeleza vipaji vya michezo nchini, na kuimarisha uwajibikaji wa kijamii kupitia michezo kwa kuongeza ajira.
TRA imesema hatua hiyo inakwenda sambamba na mifano ya timu zinazomilikiwa na mamlaka za mapato katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo michezo hutumika kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility).
Aidha, mamlaka hiyo imewaomba wadau na Watanzania kwa ujumla kushirikiana na kuunga mkono timu hiyo mpya ili kufanikisha azma ya Taifa la kujenga uchumi imara kupitia ulipaji wa kodi wa hiari.
TRA Yaimiliki Rasmi Tabora United, Yaibadilisha Jina Kuwa TRA United Sports Club

Leave a Reply