DC Msando akagua mtambo wa maji Ruvu Juu, atoa agizo kwa Mameneja Dawasa

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Albert Msando ametoa maagizo kwa watendaji wa DAWASA hususani mameneja kukomesha wizi wa mita za maji za wananchi ili kumuondolea mwananchi kero ya kulipishwa fedha kwa ajili ya kurejeshewa mita mpya.

DC Msando ametoa kauli hiyo leo Septemba 6, 2025 wakati akizungumza baada ya kufanya ziara katika mtambo wa uzalishaji maji Ruvu Juu kwa lengo la kuona na kujiridhisha hali ya uzalishaji wa maji katika mtambo huo ambao unahudumia sehemu kubwa ya Wilaya ya Ubungo, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ubungo pamoja na watendaji wa DAWASA.

Aidha, DC Msando ameridhishwa na hali ya uzalishaji maji huku akitoa maagizo kwa DAWASA kutatua changamoto zilizopo kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, pia kuhakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi bila kikwazo na kutoa taarifa kwa wakati pale panapotokea changamoto yeyote ya huduma.

Kwa upande wake, Meneja wa Mtambo wa uzalishaji maji Ruvu Juu, Mhandisi Juma Kasekwa amesema kwasasa hali ya uzalishaji imerejea katika hali ya kawaida na maeneo yaliyokuwa hayapati maji, huduma inaendelea kuimarika.

“Katika hali ya kuboresha uzalishaji maji katika mtambo wetu wa Ruvu Juu, Serikali imetupatia zaidi ya Shilingi bilioni 1 kununua pampu mbili mpya ambazo ni mategemeo yetu mpaka ifikapo mwezi Novemba tutakua tumezifunga na Kuongeza uzalishaji wa maji,” amesema Kasekwa.