Mgombea wa ubunge mteule wa chama cha Mapinduzi katika jimbo la Siha Dkt.Godwin Mollel amedai kusikitishwa na hatua ya mkutano wake kuzuiliwa masaa machache kabla ya kufanyika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Dkt.Godwin Mollel ambaye pia ni naibu waziri wa afya amesema tayari alikwisha leta jukwaa lenye gharama ya shilingi milioni 18 jambo ambalo ni hasara kubwa kwake.
Mollel amedai mkutano huo umezuiliwa kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Siha kwa madai kuwa eneo hilo ni karibu na barabara jambo ambalo anasema mikutano mingi imewai kufanyika katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Siha Christopher Timbuka amekanusha kuzuia mkutano wa kampeni ya mgombea huyo, bali eneo alilochagua halikuwa salama.
Akizungumza leo, mkuu huyo wa wilaya amesema mgombea aliweka jukwaa sehemu ambayo ni finyu na ambayo ingeweza kusababisha barabara kuu ya Sanya Juu kutopitika hali ambayo ni hatari kwa watumiaji.
Amesema walimshauri mgombea kufanyia mkutano eneo la uwanja wa ccm wilaya ambalo ni mita 20 kutoka eneo ambalo yeye alikuwa ameshaanza kusimamisha jukwaa.
Aidha amewataka wagombea kuzingatia sheria na kuangalia maeneo salama ya kufanyia kampeni na kwamba hakuna yeyote ambaye amebugudhiwa.
Leave a Reply