Mahusiano mazuri ya kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Canada umeendelea kuipaisha Sekta ya Afya nchini hivyo kuboresha zaidi ubora wa huduma za afya ngazi ya msingi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhgagama leo Julai 20, 2025 mara baada ya kumpokea Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Randeep Sarai pamoja na ujumbe aliyoambatana nao kutoka nchini Canada waliowasili kwa lengo la kufanya ziara ya siku tano (5) nchini.
“Tunaishukuru na kuipongeza Serikali ya Canada kwa kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya Sekta ya Afya nchini Tanzania, kwa mchango wanaoutoa kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Health Basket Fund) ambao unasaidia katika uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi kupitia mfumo wa ufadhili wa moja kwa moja katika vituo vya Afya awamu ya kwanza (2022–2027)” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amebainisha kuwa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Canada katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, haki za vijana balehe pamoja na kuimarisha huduma za uuguzi wakati wa kujifungua ambazo zinalenga kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga kwa kuongeza upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi.
“Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada katika sekta ya afya umeleta mafanikio mengi ikiwemo kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 43 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 1,000, kupungua kwa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai laki 100,000” amefafanua Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama hakusita kuelezea changamoto ya kasi ndogo ya kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, kutoka vifo 25 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2015 hadi vifo 24 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2022 na kutumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Canada kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza afua za afya zinazolenga kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Randeep Sarai ameshukuru kwa mapokezi mazuri nchini Tanzania na ameahidi nchi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano hasa katika Sekta ya Afya.
Waziri Sarai anatarajia kufanya ziara nchini kwa siku Tano (5) katika miradi ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali.
Leave a Reply