Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amekataa maelezo ya Mkandarasi na kumtaka aoneshe vitendo zaidi katika kazi ya utekelezaji wa mradi wa maji miji 28 Katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi; unaogharimu shilingi bilioni 22.863.
Akizungumza na Wananchi wa Mpanda baada ya kutembelea na kukagua eneo la mradi huo Mhe. Aweso amesema kuwa Serikali haitampa muda wa nyongeza mkandarasi huyo – Megha Engineering & Infrastructures Limited kwa kuwa Wananchi hawahitaji maneno bali wanataka kuona maji yanatoka kwenye mabomba.
Akiwa katika ziara hiyo, leo Tarehe 24 Julai 2025 Waziri Aweso pia alitembelea chanzo cha maji cha mradi huo ambacho ni bwawa, ambapo alieleza kuwa kazi bado hazijaanza kikamilifu na akatoa agizo kwa mkandarasi kuanza mara moja utekelezaji wa kazi katika chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, mahitaji ya maji Mpanda ni lita milioni 15 kwa siku, wakati uwezo wa sasa wa uzalishaji ni lita milioni 6. Kukamilika kwa mradi huo kutapelekea uzalishaji kufikia lita milioni 12 kwa siku, hivyo kuwezesha mji huo kuwa na jumla ya lita milioni 18 zaidi ya mahitaji ya sasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kumthibitisha CPA Rehema Nelson kuwa Mkurugenzi Kamili wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Mpanda kutokana na ufanisi aliouonyesha akiwa kaimu katika nafasi hiyo.
Leave a Reply