Waziri Mkuu Majaliwa atembelea kiwanda cha Dawa na zana za kilimo nchini Belarus

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, leo tarehe 22 Julai 2025, ameendelea na ziara yake rasmi nchini Belarus kwa kutembelea maeneo muhimu ya uzalishaji na ushirikiano wa kimkakati.

Akiwa katika mji wa Minsk, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kiwanda cha Belmedpreparaty, ambacho ni maarufu kwa utengenezaji wa dawa za binadamu.

Aidha, Waziri Mkuu pia alitembelea kiwanda cha Minsk Tractor Plant, ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa matrekta na mitambo ya kisasa ya zana za kilimo. Ujumbe wa Tanzania ulijionea teknolojia ya hali ya juu inayotumika katika uzalishaji wa vifaa hivyo.

Wakati wa ziara hiyo, pamoja na viongozi wengine, Waziri Mkuu aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Cosato Chumi.

Mheshimiwa Majaliwa pia aliweka shada la maua katika mnara wa mashujaa wa Jamhuri ya Beralus.

Kwa ujumla, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania kuimarisha mahusiano ya kimataifa kwa manufaa ya wananchi, hasa katika sekta muhimu za maendeleo kama afya na kilimo.