
Waziri wa Fedha, Mhe.Balozi Khamis Mussa Omar, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Squire, jijini Dodoma ambapo amepokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo.
Waziri Balozi Omary ameipongeza TADB kwa taarifa iliyoonesha safari ya mafanikio ya Benki, mwenendo mzuri wa mizania ya fedha na matokeo makubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo hususani katika uwekezaji na uendelezaji wa viwanda vya kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha Waziri wa fedha pia ameishauri Benki hiyo kuelekeza mipango na mikakati yao katika kuendeleza kilimo cha mazao mengine ya chakula na ya biashara yenye thamani kubwa zaidi katika soko la Kimataifa

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Frank Nyabundege, akiwasilisha taarifa za fedha na mikakati ya Benki wa kipindi cha muda wa kati (2025-2030) alisema kuwa TADB imekua kwa kasi kutoka kuwa na hesabu katika mizania ya benki (bank balance sheet) ya shilingi bilioni 362.8 (mwaka 2021) hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 (mwaka 2025).
Aidha Frank aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha, kwa kuiwezesha Benki kutimiza malengo yake kwa kuipatia mtaji huku akiiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuendelea kuiwezesha Benki hiyo kimtaji Kupitia bajeti kuu ya Serikali
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ally Munde, na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TaDB.















Leave a Reply