Wenje adai Lissu na Lema walitaka Kumpindua Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria ambaye na mtia nia wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Ezekia Wenje amekiri kuwa siku za nyuma aliwahi kuwa timu Lissu, lakini urafiki wake na Lissu ulikoma baada ya kushirikishwa kwenye kampeni ya ‘Join the Chain’ ambayo ilidaiwa kuratibiwa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini Godbless Lema, iliyolenga kuupindua uongozi wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe.

“Ni kweli mimi nilikuwa timu Lissu, na kwanini nilitoka? Mimi nilikimbia nchi, na hata Godbless Lema alikimbia nchi, vilevile Tundu Lissu. Uzoefu wa kukimbia nchi sio mdogo kwamba unakwenda nchi ambayo hujui hata mila na desturi zao..sasa tukiwa huko mambo yakawa mengi mpaka Mwenyekiti Freeman Mbowe akakamatwa akiwa gerezani.

“Wakati Mwenyekiti akiwa gerezani marafiki zangu hawa wakashauriana waanzishe kitu kinachoitwa ‘Join the Chain’ na Mwenyekiti aliyeasisi hilo vuguvugu ni rafiki yangu Godbless Lema. Join the Chain lengo lake lilikuwa ni kuwa ikusanywe fedha, iitishe Baraza Kuu na mwisho wake Mkutano Mkuu, lengo kubwa kutokana na vikao tulivyofanya..kwasababu waliamini kabisa kwamba Freeman Mbowe ana kesi ya ugaidi, waliamini kabisa hawezi akatoka gerezani. Kwahiyo ikaitishwa Join the Chain, fedha zote za vuguvugu hilo muulizeni Godbless Lema ziko wapi, ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya Join the Chain.

“Walikuwa wanaamini hawezi kutoka ili waende wakafanye mapinduzi kwenye chama, Tundu Lissu awe Mwenyekiti wa chama, Peter Msigwa awe Makamu Mwenyekiti wa chama, niliposhirikishwa kwenye mambo kama hayo, mimi nilikataa uasi na hiki ndicho chanzo cha ugomvi mkubwa kati yangu na marafiki zangu, nikajiondoa kwenye mchakato wote huu wa Join the Chain,” amesema Wenje.