Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa shukrani zake za dhati kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho kwa kumteua kuwania nafasi ya Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akitoa shukrani hizo, Dkt. Samia alisema, “Shukrani za dhati kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama chetu, chama kinachobeba mustakabali wa Taifa letu na imani ya Watanzania. Uamuzi wenu ni sauti ya mamilioni ya Watanzania wanaothamini matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM.”
Dkt. Samia ameahidi kuendeleza juhudi za maendeleo na ustawi wa Watanzania wote kwa nguvu, akili na maarifa yake yote, akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuwatumikia wananchi kwa moyo safi na wa dhati.
“Ahadi yangu ni kuendelea na kazi njema ya kuitumikia nchi yetu na Watanzania wote kwa nguvu zote, akili na maarifa yangu yote, wakati wote,” aliongeza Dkt. Samia.
Pia, alimuomba Mwenyezi Mungu kuendelea kuliweka taifa katika amani na ustawi, huku akisisitiza mshikamano ndani ya chama kwa kauli yake ya “Kidumu Chama Cha Mapinduzi.”
Leave a Reply