Na Kelvin Lyamuya
Ili makala hii ieleweke vyema, lengo la mwandishi halipo katika kuidhihaki Taasisi kubwa ya soka Tanzania ambayo ni Yanga. Ujumbe uliopo humu unaelezea vyema namna Ligi ya Tanzania ilivyokuwa daraja kwa makocha wenye CV za kawaida kwa ajili ya kujipata zaidi kwenye soka la Afrika.
Tumeshuhudia Nasredine Nabi akiondoka katika mitaa ya Twiga na Jangwani na kuhamisha benchi lake la ufundi hadi mitaa ya Naturena, Johannesburg nchini Afrika Kusini ambako hivi sasa anainoa timu kongwe katika Ukanda wa Kusini, Kaizer Chiefs.
Kama sio rekodi ya kuipeleka Yanga fainali ya Shirikisho Afrika miaka 2 iliyopita sambamba na makombe mawili mfululizo ya Ligi Kuu na takwimu ya kibabe ya kucheza mechi zaidi ya 40 mfululizo bila kupoteza, ingekuwa ngumu sana Mzee Nabi kuingia kwa Madiba au hata kugusa timu ya ngazi ya juu kama ilivyo Kaizer.
Na Gamondi katembea humohumo, ujio wake Yanga ulikuwa ni kwaajili ya kuiendeleza timu katika mafanikio ya ndani na akaweza. Ingawa viongozi walimuondoa ghafla kufuatia yale matokeo ya vichapo kutoka kwa Azam na Tabora Utd lakini, timu kubwa zilizomfuatilia katika ubingwa wa 30 wa Yanga hazitaacha kumtamani.
Mitaa ilisemaje kuhusu kuondoka kwa Gamondi? Kila mmoja alitabiri anguko la Yanga. Kila mmoja aliiona Yanga ikipungua nguvu kwa asilimia kubwa. Wengi hawakuiona Yanga ikifanya maajabu yoyote baada ya kuondoka kwake. Na leo hii Yanga imeshindwa kutinga Robo Fainali huko CAFCL na wasiwasi ni mkubwa sana miongoni mwa Wananchi.
Hata hivyo, ndio maisha ya mpira wa miguu. Kwa kocha, kuajiriwa na kufukuzwa ni kawaida. Kwa timu, kushinda na kuanguka pia ni desturi. Muhimu mambo mengine lazima yaendelee.
Kwa sasa Gamondi hatuwezi kujua hisia zake huko aliko. Kimsingi, hisia zake hazituhusu. Tunachokitazama sisi watu wa soka ni rekodi zake zitaendea kupaa au kuporomoka. Hicho ndio tunachosubiri kuona.
Mzee Nabi tunafahamu huko Kaizer Chiefs aliko hali ni tete na hii ni kutokana na ubora na mahitaji tofauti ambayo ameenda kukutana nayo huko. Kwa maana, ligi ya Afrika Kusini kwa sasa ni ya 6 kwa Ubora Afrika nyuma ya Ligi yetu ambayo imepanda hadi nafasi ya 4 kwa mujibu wa orodha mpya ya IFFHS iliyotolewa hivi karibuni.
Nabi aliondoka Tanzania akiwa bora na pia rekodi zilimpa nguvu ya kutoboa katika ligi yoyote Afrika ukiondoa kule Kaskazini ambako standard ni kubwa sana. Kaizer yake iko nafasi ya sita kwenye ligi, nyuma ya vinara Mamelodi kwa tofauti ya alama 6, marekebisho machache kwenye timu yake yatasaidia kupanda zaidi.
Unaona namna maisha ya Nabi yanavyokuwa na changamoto zaidi ni kwa sababu ametoka kwenye ligi yenye changamoto pia, sasa vipi kuhusu Gamondi ambaye yeye kutokana na presha klabu ikamuondoa, kwa maana klabu ya Yanga haifikirii tu hapa, ina mipango mikubwa ambayo inahitaji kwenda sawa na kasi ya maendeleo ya soka.
Ukitazama hata taarifa za klabu ambazo zinawania saini yake mfano RAJA Casablanca na AS FAR Rabat utagundua Gamondi ana nafasi nyingine ya kuongeza CV yake na pia kupaa zaidi katika rekodi za Afrika. Kitu ambacho kitachochea maumivu katika kidonda kibichi ambacho mashabiki wa Yanga bado wanacho tangu kocha huyo aondolewe bila mategemeo yao!
Kwanini Gamondi awe chumvi katika kidonda cha Yanga? Kwa sababu iwapo angevumiliwa timu hii ingevuka makundi CAFCL na huo ni ukweli mchungu. Hata hivyo, hayo mambo yamepita na Yanga wana nafasi nyingine ya kuweka rekodi zao sawa kwa maana ya kupambana kwenye Ligi Kuu.
Kwa sasa Gamondi bado hajapata timu licha ya mtifuano mkali ulioibuka kati ya RAJA na AS FAR Rabat ambazo zilikuwa zinamgombania. Baada ya mazungumzo na klabu hizo kugonga mwamba, mapema mwezi huu ilitaarifiwa kwamba Gamondi amejiunga na kampuni ya usimamizi wa michezo ya X07 Sports Management yenye maskani yake Lisbon, Ureno.
X07 Sports Management ni kampuni ya mawakala wa michezo inayomilikiwa na Mohamed Rezki na Rui Gomes na hao ndio watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mkufunzi huyo anapata ofisi mpya ya kuendeleza ubora wake kama kocha.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.