ZRA Yavunja Rekodi Ya Makusanyo, Wafikisha Bilioni 81 Makusanyo Ya Januari 2025

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imefanikiwa kukusanya bilioni 81.512 ambapo ni ufanisi wa asilimia 100.65 ya kiasi kilichokadiriwa kukusanywa kwa mwezi Januari mwaka 2025 cha shilingi bilioni 80.984 na kufanya makusanyo hayo kuwa ni ya kihistoria katika ukusanyaji wa mapato ambayo yamewahi kukusanywa na ZRA.

Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamkala ya Mapato Zanzibar (ZRA) Said Ali Mohammed ameeleza hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Ofisini kwake Mazizini.

Amesema makusanyo ya mwezi Januari mwaka 2024 yalikuwa ni shilingi bilioni 70.180 yakilinganishwa na makusanyo ya mwezi Januari mwaka huu yameonesha ogezeko la makusanyo ya bilioni 11.332 sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 16.15.

Akizungumzia sababu zilizopelekea kufanya vizuri kwa mwezi huo alisema ni juhudi zinazofanywa na viongozi wakuu wa nchi kwa kuweka mazingira bora yanayovutia uwekezaji mkubwa unaonendelea kufanyika Zanzibar kwani kutokuwepo kwa mazingira bora uwekezaji ungekuwa hafifu na mapato yasingeweza kupatikana.