Tanzania na utajiri wa soka la wanawake wanaokipa nje ya nchi 

MIAKA zaidi ya 10 imekwishapita tangu nilipokuwa nikimsikiliza nguli wa Habari za Michezo na Uchambuzi, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ akiuelezea Mpira wa Miguu wa Wanawake kupitia mawimbi ya redio na kiukweli mwamba huyo ndiye aliyenisaidia kuelewa kiundani upande huo wa pili wa shilingi.

Kwa wale waliokuwa wakimfuatilia Maestro tangu akiwa kituo cha redio cha Clouds FM ndani ya kipindi cha Sports Extra, wanafahamu jinsi alivyotumia sauti yake vyema kuwaelezea kwa utulivu wakongwe wa soka la wanawake duniani.

Kuanzia akina Abby Wambach, Carli Lloyd, Marta da Silva, Mia Hamm, Birgit Printz na wengineo wengi ambao mkongwe huyo aliweza kuwafafanua kwa undani na hapo ndio ukawa mwanzo wa mimi kujua ni kwa kiasi gani soka la wanawake lilivyokita mizizi.

Kwa faida ya wengi, mizizi ya soka la hawa dada zetu ilianza kusambaa rasmi miaka ya 1920 huko United Kingdom na mechi ya kwanza iliwavutia mashabiki wengi kiasi cha kuujaza uwanja ambao ulikuwa na uwezo wa kupokea watazamaji 50,000. 

Hata hivyo, mwanzo huo haukuwa mzuri sana kufuatia Chama cha Soka England (‘Football Association’ au ‘FA’) kupiga marufuku wanawake kusakata kabumbu nchini humo kuanzia mwaka 1921 hadi 1970.

Kiujumla, sio England tu ambako mchezo wa soka uliruhusiwa kuchezwa na wanaume pekee bali hata kwa baadhi ya mataifa mengine nako kulitokea changamoto kwa wanawake kutoruhusiwa kucheza mchezo huo.

Mnamo miaka ya 1970 soka la wanawake lilifufuliwa upya kutokana na mashindano tofauti ya kimataifa yaliyochochea kurudishwa kwake katika ramani ya michezo duniani. 

Hata hivyo, bado upande huo wa pili haukuwa na sauti ambayo ingewawakilisha katika meza kuu ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) hadi mwaka 1986 alipoibuka mwanamama Ellen Wille ambaye cheo chake cha uongozi wa Shirikisho la Norway ndio kilimpa nguvu ya kuwahoji FIFA juu ya sababu za kuwapotezea wanawake katika mchezo wa soka.

Huo sasa ukawa ndio mwanzo wa soka la wanawake kupewa uzito mkubwa na hatimaye mashindano ya kwanza ya Kombe la Dunia kwa Wanawake yalipochukua nafasi mwaka 1991 na yalichezwa nchini China.

Baada ya wanawake kuishinda vita ya kwanza ya kupambania soka lao kupewa uhuru kama ilivyo kwa wanaume, vita ya pili ilikuwa ni kupata uwezo wa kuonekana na kusikika duniani kote.

Kwa muda mrefu vyombo vya habari vilijitahidi kuutangaza mpira wa miguu wa wanawake na hadi kufikia 2015 dalili zilishaanza kujitokeza juu ya ufuatiliaji mkubwa wa soka lao kama ilivyoshuhudiwa katika fainali nyingine za Kombe la Dunia kwa wanadada mwaka huo. 

Mwaka 2019, rekodi kubwa iliwekwa katika michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake ambapo watu bilioni 1.12 walitajwa kuwa ndio waliotazama fainali hizo zilizochezwa katika mataifa mawili kwa wakati mmoja, Australia na New Zealand.

Kipindi hicho dada zetu hapa Tanzania tayari walikuwa katika msingi mzuri na tayari walishaonja mafanikio ya ubingwa kwenye mashindano ya ndani ya Bara la Afrika kuanzia CECAFA (2016,  2018) wakiwa na mastaa kama vile Stumai Abdallah, Asha Rashid na Mwanahamisi Omary.

Ambapo mastaa hao pia ndio walioipa timu ya Taifa ya Tanzania Wanawake ‘Twiga Stars’ kombe la COSAFA 2021 wakiwa na chipukizi kadhaa ambao utawafahamu vyema kupitia makala hii;

NOELA PATRICK (ISRAEL)

Beki huyo kwa sasa anakipiga huko nchini Israel katika timu ya wanawake ya ASA Tel Aviv ambayo inasimamiwa na Chuo Kikuu cha Tel Aviv na ni sehemu pia ya klabu ya michezo ya ASA Tel Aviv.

Timu hiyo ya wanawake ina rekodi ya kubeba makombe 8 ya ligi ya wanawake nchini Israel ijulikanayo kama Ligat Nashim na pia wana mataji matano ya Israeli Women’s Cup, huku ikiwa imewahi kushiriki mashindano ya UEFA kwa upande wa wanawake, ambayo ni mashindano ya ndoto za wachezaji wengi duniani.

Timu hiyo ilikuwa ni moja kati ya vikosi vya kwanza vya soka la wanawake kuanzishwa Israel chini ya mpango maalum wa Shirikisho la Soka Israel (IFA) na ndio timu pekee ambayo inacheza Ligi Kuu tangu ilipoanzishwa, ikionesha namna gani ambavyo Noela ametua kwenye klabu yenye uzoefu wa kutosha wa soka la ushindani.

Kiujumla huu ni msimu wa 24 kwa klabu hiyo kucheza katika ligi ya Israel na ukiacha rekodi ya mataji nane, pia wameweza kushika nafasi ya pili kwenye ligi kwa idadi ya mara saba.

Mara yao ya kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wanawake ilikuwa ni msimu wa 2010–11, lakini katika mashindano hayo walifanikiwa kuvuka raundi ya awali mara moja tu mnamo msimu wa 2011-12 na kufika hadi raundi ya 32 ambapo waligomga mwamba dhidi ya kikosi cha Torres Calcio Femminile.

ASA Tel Aviv pia wana rekodi ya kucheza fainali 11 za Israeli Women’s Cup, wakipoteza saba za awali zikiwemo fainali sita mfululizo kati ya 2004 na 2009. Lakini walifanikiwa kubeba kombe la kwanza 2011 na yakafuatia mengine 2012 na 2014.

SUSAN ADAM (MISRI)

Mlinzi mwingine machachari huyu wa Twiga Stars ambaye amehamisha maisha yake ya soka hadi nchini Misri katika klabu ya wanawake ya FC Masar ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Tutankhamun FC, ikiwa na makazi yake jijini Cairo na inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini humo.

Klabu hiyo anayoitumikia Susan, iliibuka rasmi katika ramani ya soka la wanawake mnamo mwaka 2019 na ilipofika mwaka 2021 ndipo walipofanikiwa kupata mmiliki ambaye ni mfanyabiashara mkubwa Misri, Sir Mohamed Mansour kupitia kampuni yake ya Right to Dream Egypt.

Huyo ndiye aliyeibadili jina klabu hiyo mwaka jana (2024) kutoka Tutankhamun hadi kuiita FC Masar.

Mwaka huo ndio ulikuwa wa kwanza katika historia yao, kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake (CAF Women’s Champions League) wakiandika rekodi husika mnamo Oktoba 15, 2024 na zaidi walifanikiwa kumaliza kama washindi wa tatu kufuatia ushindi wa mikwaju ya penati dhidi ya Edo Queens F.C. 

Rekodi yao katika soka la Misri ni pamoja na kufanikiwa kubeba kombe moja la Ligi Kuu ya Wanawake (2024) na Kombe la Egyptian Women’s Cup mara mbili mfululizo (2023, 2024).

Susan hayuko peke yake katika ligi ya Wanawake nchini Misri, kwani yupo nyota mwingine anayejulikana kama Maimuna Mussa, mlinzi mwingine anayeitumikia klabu changa ya ZED FC Women.

OPAH CLEMENT, JULITA SINGANO (MEXICO)

Akiwa na umri wa miaka 24, Opah Clement tayari ana hadhi kubwa katika historia ya maisha yake ya soka, akiwa ndiye nahodha mkuu wa Twiga Stars kwa sasa na klabu anayoitumikia ni Juarez ya nchini Mexico.

Klabu hiyo anayoitumikia Opah ilianzishwa katika msimu wa 2019-20 kwa ajili ya kuanza kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake Mexico (Liga MX Femenil) na zoezi zima la kuihalalisha lilianzia katika ununuzi wa haki zote za ilivyokuwa timu ya soka ya Lobos BUAP ambayo ilijiondoa kwenye rekodi za mpira wa miguu mnamo Juni 11, 2019.

Na hapo ndipo ukawa mwanzo wa timu ya wanawake ya Juarez ambayo kwa Opah ni klabu ya tano kuitumikia baada ya Simba Queens (2019–2022), Kayseri Kadin (2022), Besiktas (2023-24), na Henan Jianye (2024).

Julita Singano nae ni staa wa Twiga Stars aliyeko nchini Mexico na yeye anaitumikia klabu hiyohiyo ya Juarez, akicheza katika nafasi ya ulinzi.

CLARA LUVANGA (SAUDI ARABIA)

Alipo Cristiano Ronaldo na Sadio Mane ndipo Clara Luvanga anakotafutia ugali wake, akiwa ni mmoja kati ya wanasoka wa kike wachache sana kutoka Tanzania aliyebahatika kucheza ndani ya taifa lililokusanya masupastaa wa kutosha.

Ikijulikana kwa jina la utani Sayidat Al-Aalami kwa maana ya ‘Wanawake wa Kimataifa’, Al Nassr inajivunia kuwa na mshambuliaji huyo machachari ambaye anawakilisha historia nzuri ya kuwa na wachezaji hodari wanawake, wenye uwezo wa kufanya makubwa Saudi Arabia na barani Asia kwa ujumla.

Hadi sasa, Luvanga amekuwa akitamba katika rekodi zote za wafungaji bora wa muda wote katika timu ya wanawake Al Nassr, akifunga zaidi ya mabao 15 katika jumla ya mashindano matatu tofauti kuanzia Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Asia na Kombe la Saudia (SAFF Women Cup).

Kiujumla, Al Nassr hadi wakati huu inatamba na makombe matatu; mawili ya ligi kuu (2022-23, 2023-24) na moja la SAFF walilobeba msimu wa 2021-22, yakiwa ndio makombe pekee waliyoweza kushinda katika kipindi cha miaka saba tangu ilipoanzishwa.

ENEKIA KASONGA (MEXICO)

Silaha nyingine hatari ya Twiga Stars yenye rekodi ya kushinda tuzo Mchezaji Bora wa mashindano ya COSAFA U-20 (2019) bila kusahau tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Morocco msimu wa 2021/22 na hivi sasa ni mchezaji halali wa klabu ya soka ya wanawake ya Mazatlan inayoshiriki ligi ya soka ya Mexico.

Mazatlán Futbol Club Femenil ilianzishwa mnamo Juni, 2020, ikihamishwa mji kutoka Sinaloa hadi Mazatlán na rasmi kuwa klabu ya soka ya wanawake ambapo katika kipindi cha miaka mitano hadi sasa bado hawajaweza kubeba kombe.

Mategemeo yao makubwa yapo kwenye miguu ya kinda Enekia ambaye rekodi yake ya kutisha ya kufunga mabao zaidi ya 100 katika klabu za Alliance FC, Ruvuma Queens, Ausfaz Assa-Zag, Kryvbas Kryvyi Rih na Eastern Flames ndio iliyowavutia hadi kumsajili.

AISHA MASAKA, MALAIKA MEENA (ENGLAND)

Taifa lenye umaarufu mkubwa wa soka la ngazi ya klabu duniani ni England na mabinti hao wawili wamebahatika kutua nchini humo kwa ajili ya kusaka maisha zaidi katika mchezo huo, mmoja akicheza Ligi Kuu ya Wanawake (Women Super League) na mwingine akikichafua Ligi Daraja la Kwanza (Women Championship).

Masaka ambaye aliwahi kuitumikia timu ya wanawake ya Yanga Princess, ndiye anayecheza ligi kuu ya England akiwatumikia waajiri wake Brighton and Hove Albion ambayo ilimsajili mwaka jana wa 2024 akitokea BK Hacken ya Sweden baada ya kuonesha uwezo mzuri huko.

Ana uwezo wa kucheza nafasi zote katika safu ya mashambulizi na anatajwa kama mmoja wa wanasoka wa kike kutoka Tanzania watakaofika mbali zaidi kutokana na jitihada zake zisizo na kikomo.

Jina lingine ambalo ni geni kwa wadau wengi wa soka la Wanawake Tanzania ni Malaika Meena, kiungo hodari ambaye historia ya maisha yake ya soka inavutia na kuibua matumaini makubwa kwamba atakuwa msaada katika kikosi cha Twiga Stars.

Nyota huyo kwa sasa anaitumikia Bristol City ambayo inashiriki Women Championship ambako alisaini kandarasi ya miaka miwili na nusu baada ya kusajiliwa Januari mwaka huu.

Kiungo huyo aliwahi kupita katika akademi za soka za Arsenal na Chelsea kabla ya kutimkia timu ya soka ya Wake Forest University iliyopo North Carolina, Marekani.

Malaika alidumu hapo kwa muda wa miaka mitatu na nusu kabla ya kurejea England.

Nyota wengine wanaokipiga nje ya Tanzania ni Rehema Ramadhan (Rwanda), Mariam Yusuf (Burundi) na Diana Lucas (Uturuki).