Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa imemhukumu kifungo cha miaka minne jela Mzee Chezali Kambole (74) Mkazi wa semtema kwa kosa la kumchoma na kitu chenye ncha kali Filbert Bai (32) anayedaiwa kuwa mdeni wake mkazi wa mtaa huo wa semtema uliopo Manispaa na Mkoa wa Iringa.
Hukumu hii ya kesi ya kuua bila kukusudia imesomwa na Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, upande wa jamhuri ukisimamiwa na wakili Habati Ishengoma pamoja na Majid Matitu huku upande wa mshtakiwa ukiwakilishwa wakili Jerry Mungo pomoja na Asifiwe Mwanjero.
Imeelezwa mahakamani hapo mshtakiwa ambaye alikuwa akijishughulisha na kazi ya kuuza mipini ya jembe alikuwa akimdai Marehemu fedha kiasi cha shilingi Elfu mbili, siku ya tukio wakiwa kilabuni wanakunywa pombe alikumbushia deni lake na Marehemu anadaiwa kukataa kulipa huku akijibu ‘Silipi’.
Baada ya majibizano ya muda Mzee Kambole akaanza kumpiga Marehemu sehemu mbalimbali za mwili wake kisha akachomoa kisu na kumchoma sehemu ya kushoto ya kifua hali iliyopelekea kuvuja damu nyingi na kupelekea umauti wake.
Hata hivyo Mshitakiwa alipopewa nafasi yakujitetea alikiri kutenda kosa hilo huku akiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na alikuwa katika hasira iliyochanganyana na ulevi huku akigusia umri wake wa uzee wa miaka 74 na ni tegemeo kwa Familia yake.
Hata hivyo upande wa jamhuri ukiongozwa na wakili Habati Ishengoma uliendelea kupigilia msumari Mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kutokana na historia mbaya iliyopo katika jamii hasa kwa baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi.
“Kwa umri wa Mzee Kambole tulitegemea awe na busara kwani Marehemu alikuwa sawa na mjukuu wake kitendo cha kumshambulia na kufanya maamuzi ya kumchoma na kisu hayakuwa na busara kwani kipindi chote Marehemu hakuonesha hali ya kujitetea hata baada ya kutenda kosa alikimbia hivyo alijua dhahiri alichokuwa anakifanya na ikumbukwe Uhai wa Marehemu haufanani na shilingi Elfu mbili aliyokuwa anaidai Mzee Kambole ” Alisisitiza Wakili Ishengoma
Baada ya ku kusikiliza pande zote mbili ndipo mahakama ikamkuta Mzee Kambole kuwa na hatia ya kuua bila kukusudia ambayo ni kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha sheria ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, huku ikijibu utetezi wa kuwa alikuwa amelewa haukuwa na mashiko kabisa.
“Adhabu ya kosa hili ni kutumikia kifungo jela si chini ya miaka 10 hivyo mahakama imetumia busara hasa kutokana na umri wako, hauna historia ya kutenda makosa, pia majukumu yako hivyo inakuhukumu kwenda jela miaka minne, utetezi wako kuwa ulilewa haukuwa na mashiko kama ulilewa uliwezaje kukumbuka kiasi cha deni, mdeni wako, ulikumbukaje ulipo weka kisu na kwanini baada ya kutenda kosa ulikumbuka kuwa kuna kukimbia kwa maana hii inaonesha kiasi cha pombe ulichokunywa hakikuathiri ubongo wako hadi ufikie maamuzi hayo” Alisema Jaji Mwipopo
Leave a Reply